WAKATI sehemu ya makaburi imekuwa ikiogopwa na watu wengi kutokana na
ukweli kwamba ni makazi ya wafu, hali ni tofauti kwa mtoto wa kiume
anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 8-9 ambaye jina lake
halikuweza kufahamika, kuishi katika makaburi ya Kigilagila, Yombo
jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio na baadaye kufuatiliwa
kwa karibu na waandishi wetu, zinasema mtoto huyo ambaye hafahamiki
alikotokea, alionekana akishinda na kulala katika makaburi hayo kwa
zaidi ya mwezi mzima uliopita, kabla ya kutoweka kuelekea sehemu
isiyojulikana.
Lakini baada ya siku kadhaa za kutoweka kwake, majirani wanasema
walimuona tena mtoto huyo akiendelea na maisha eneo hilo ndipo walitoa
taarifa Kituo Kidogo cha Polisi Yombo kuwataarifu juu ya tukio hilo
lisilo la kawaida.
Polisi walifika makaburini hapo na kumchukuwa kijana huyo lakini
walipomuhoji hakuweza kuongea chochote, hali iliyowafanya askari hao
kutojua cha kufanya.
Kutokana na hali hiyo, polisi wa Kigilagila walifanya mawasiliano na
Kituo cha Buguruni kwa hatua zaidi, ikiwemo kubaini anakotoka na sababu
za kuishi katika mazingira hayo.
Gazeti hili lilifika na kumkuta mtoto huyo akiwa katika Kituo cha
Buguruni anakohifadhiwa wakati ndugu au wazazi wakisubiriwa, kabla ya
taratibu za kumkabidhi kwa Ustawi wa Jamii kuanza kuchukuliwa.
Aidha, vyanzo vyetu ndani ya kituo hicho vilisema kuna watu
walijitokeza wakiwa wanatafuta mtoto wa namna hiyo, lakini baada ya
kumuona, walisema hakuwa yeye.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, SACP Marietha Minangi
alithibitisha kuwepo kwa mtoto huyo na kwamba taratibu zinafanywa ili
kulimaliza tatizo lake.
“Natoa wito kwa wananchi waliopotelewa na kijana mwenye umri huo,
kufika katika Kituo cha Polisi Buguruni ili kuweza kumtambua mtoto
huyo,” alisema Kamanda Minangi.
credit: vituko vya mtaa
0 comments:
Post a Comment