Find Us On Facebook
 
X

Monday, 20 January 2014

UJANGILI WAZIDI KUZUA HOFU, ANGALIA PICHA MAJANGILI YALIVYOMUUA FARU ALMAARUFU KAMA "MAMA SERENGETI"...!!!


Faru akiwa ameuawa mbugani.

Kasi ya ujangili imeendelea kuleta hofu dhidi ya rasilimali nchini, baada ya juzi majangili kuua faru aitwaye ‘Mama Serengeti’ na kumng’oa pembe zake katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Aidha, kundi jingine linalosadikiwa kuwa la majangili, likiwa ndani ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro lilivamia basi la abiria na kuwapora wasafiri fedha na mali zao juzi alasiri.
Kutokana na hali hiyo, Serikali jana alfajiri ilituma kikosi maalumu cha askari 20 wenye silaha na vifaa maalumu vya kupambana na ujangili ili kuongeza nguvu na kuhakikisha majangili hao wanatiwa mbaroni.
Hayo yamethibitishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, huku akisisitiza kuwa, hali ya ujangili nchini ni mbaya na kwamba, kwa namna yoyote ile Serikali itapambana na vitendo hivyo vya uhujumu uchumi vinavyofanywa dhidi ya rasilimali za Taifa.
“Tumeagiza kila gari ama mtu anayeingia na kutoka katika hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro apekuliwe, ikiwa ni sehemu ya kuwasaka wahalifu, tahadhari imetolewa kwa mwananchi yeyote kutoa taarifa zinazohusu wageni na watu wanaotiliwa shaka, tuna taarifa ya raia watatu wa nchi moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hivyo kuonesha dalili kuwa mtandao wa kuua faru ni mkubwa,” alisema Nyalandu.
Akielezea ilivyokuwa, Nyalandu alisema walipokea taarifa za kusikitisha usiku wa kuamkia jana, saa 6.30 za majangili kuua faru katika eneo la Moru, Kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kwamba askari wa wanyamapori waliokuwa doria ndio waliogundua faru huyo akiwa amepigwa risasi na pembe zake kung’olewa.
Faru huyo ameacha mtoto mwenye umri wa miezi miwili na mpaka taarifa hiyo ilipotolewa, mtoto huyo alikuwa hajulikani alipo. Inaelezwa alipewa jina Mama Serengeti kutokana na kuwa chimbuko na faru wengine 31 `wazalendo’ waliobaki katika Hifadhi ya Serengeti.
Mbali ya faru hao `wazalendo’, hifadhi hiyo pia ina faru wengine wanne kati ya watano ambao waliletwa nchini kwa mradi maalumu uliosimamiwa na Rais Jakaya Kikwete kutoka Afrika Kusini. Faru mmoja kutoka Afrika Kusini aliuawa na majangili Desemba mwaka 2012.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, baada ya kupokea taarifa, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ilichukua hatua ya dharura kuagiza msako wa majangili katika maeneo yote yanayozunguka hifadhi hizo mbili.
“Serikali inawasaka kwa udi na uvumba raia hao watatu na wananchi wanaombwa kusaidia kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama, sambamba na hatua hiyo, mapema leo (jana), wizara imetuma kikosi maalum (Rapid response team) cha askari 20 wakiwa na silaha na vifaa maalumu ili kuongeza nguvu na kuhakikisha majangili wanapatikana,” alieleza Nyalandu.
Akielezea hatua nyingine zilizochukuliwa katika mapambano dhidi ya ujangili, Nyalandu alisema serikali katika kutekeleza maazimio ya Bunge yaliyotolewa na Kamati ya James Lembeli, Mbunge wa Kahama (CCM), imechukua hatua mahususi ikiwa ni pamoja na kutekeleza agizo la Rais Kikwete la kuundwa kwa Tume ya Kimahakama kuchunguza tuhuma dhidi ya operesheni tokomeza.
Nyalandu alisema baada ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika operesheni hiyo, serikali itaendesha operesheni nyingine. Lakini wakati ikijiandaa kwa `vita’ nyingine kali dhidi ya majangili, alisema wizara imewasimamisha kazi watumishi 23 wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kula rushwa na kusaidia majangili.
Alisema pamoja na taarifa za kukamatwa kwa meno ya tembo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo tukio lililoripotiwa katika Bandari ya Dar es Salaam mapema mwezi huu, wiki iliyopita, katika Kijiji cha Ugenza, Mufindi, waliwakamata majangili watatu wakazi wa Dar es Salaam wakisafirisha meno ya tembo kilo 37.
Aliwataja waliokamatwa na maeneo wanakoishi kwenye mabano kuwa ni mwanamke mmoja ambaye ni Salome Aloyce (Sinza Madukani), Rajabu Omari (Kigogo) na Kadili Kisanduku (dereva teksi wa Mbezi Louis). Alisema walikuwa na gari aina ya Toyota Corona yenye namba za usajili T580 ABL, mali ya Florian Elias wa Dar es Salaam na walikuwa wanaelekea jijini humo. Sasa wanashikiliwa na Polisi.
Katika kipindi cha miaka mitatu (2008 hadi 2013), meno ya tembo yenye uzito wa kilo 32,987 yalikamatwa ndani na nje ya nchi, jambo lililo ishara ya kukithiri wa ujangili wa wanyama hao nchini.
Mwaka 2010, Tanzania ilipigiwa mstari mwekundu kuwa moja ya nchi iliyoathirika zaidi kwa ujangili na biashara ya meno ya tembo duniani. Idadi ya tembo inaelezwa kupungua nchini kwa kasi ambapo mwaka 2009 kulikuwa na tembo 109,000 lakini kutokana na ujangili, walifikia 70,000 mwaka 2012.

0 comments:

Post a Comment