Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen
wamekubaliana kuvunja mkataba katika makubaliano ambayo ni siri kwa
pande zote mbili.
Uamuzi huo umetangazwa leo (Februari 27 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam kwa pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Kocha Poulsen mbele
ya waandishi wa habari.
Rais Malinzi kwa niaba ya TFF ametoa shukrani za dhati kwa Kocha
Poulsen kwa ushirikiano na mchango ambao ameutoa kwa Tanzania kuanzia
kwenye mpira wa miguu wa vijana.
Naye Kim amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompatia kwa
kipindi cha miaka mitatu alichokaa nchini kuanzia Mei 2011 alipoteuliwa
kuwa kocha wa timu za Taifa za vijana, na baadaye Taifa Stars.
Akizungumzia benchi jipya la ufundi la Taifa Stars, Rais Malinzi
amesema linatarajiwa kutangazwa hivi karibuni likiongozwa na kocha
kutoka nje ya Tanzania.
Amesema kwa upande wa mechi dhidi ya Namibia itakayochezwa Machi 5
mwaka huu jijini Windhoek, Stars itaongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa
Ufundi, Salum Madadi akisaidiwa na kocha Hafidh Badru kutoka Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Kocha Madadi amewaondoa wachezaji watano wa
Yanga katika kikosi kilichotajwa awali ili wapate fursa ya kuitumikia
timu yao kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly
ya Misri.
Wachezaji hao ni Athuman Idd, David Luhende, Deogratius Munishi,
Frank Domayo, Kelvin Yondani na Mrisho Ngasa. Pia kipa Ivo Mapunda
ameondolewa katika kikosi hicho baada ya kupata msiba.
Nafasi zao zimezibwa na wachezaji Abdi Banda (Coastal Union), Himid Mao
(Azam), Juma Luizio (Mtibwa Sugar), Said Moradi (Azam) na Shabani Kado
(Coastal Union).
Taifa Stars itaingia kambini keshokutwa (Machi 1 mwaka huu) jioni
kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam, na itaondoka Machi 3
mwaka huu alfajiri kwa ndege ya South African Airways na kurejea nchini
Machi 7 mwaka huu saa 8.15 mchana.
Thursday, 27 February 2014
Taarifa kuhusu kocha wa Taifa Stars kuachishwa kazi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment